SERIKALI kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imeahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wazalishaji, wafanyabiashara na wenye viwanda ili kukuza uchumi wa nchi, ikiwa ni pamoja na kusimamia maendeleo ya viwango na ubora wa bidhaa zinazozalishwa katika sekta mbalimbali na viwandani.

Hatua hiyo inalenga kutimiza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amedhamiria kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara nchini, kwa kuboresha mifumo ya uratibu na usimamizi wa utekelezaji wa mipango, mikakati na program mbalimbali za kisekta ili kufikia malengo ya kiuchumi na kijamii ya maendeleo endelevu na ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.

Hayo yalisemwa juzi (Novemba 30) Makao Makuu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) jijini Dar es Salaa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani.

Alisema sekta ya viwanda na biashara ni moja ya mihimili mikubwa katika kukuza uchumi wa nchi na kuchangia katika pato la Taifa, kutokana na bidhaa za viwandani zinazozalishwa na kuuzwa ndani na nje ya nchi, pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania.

Kutokana na umuhimu huo, Dkt. Abdallah, aliwataka wadau wote kila mmoja katika nafasi yake kuendelea kushirikiana na TBS, kwa kutoa msaada na uzoefu katika taaluma yake ili kuchangia ipasavyo katika utengenezwaji wa viwango nchini, kwani TBS ni moja ya mashirika ya umma bora yanayoheshimika nchini, ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na Afrika nzima

Dkt. Abdallah, alisema TBS imekabidhiwa mamlaka ya kutengeneza na kusimamia utekelezaji wa viwango nchini, kwani viwango ni muhimu katika kuendeleza sekta ya viwanda na biashara nchini.

Alitoa rai kwa wadau na wananchi kwa ujumla kushiriki na kutoa maoni katika mchakato wa uandaaji na utengenezaji viwango ili vikidhi mahitaji ya jamii yetu.

Akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani, Dkt. Abdallah, alisema ni muhimu kwani ni njia mojawapo ya kuenzi juhudi shirikishi za maelfu ya wataalamu duniani ambao hutengeneza mikataba ya hiari na lazima ya kiufundi ambayo huchapishwa kama viwango vya kitaifa na kimataifa ili kulinda afya za walaji na mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya alisema wanatambua juhudi za wadau na mchango mkubwa wa kujitolea katika kuandaa viwango na hatimaye kuhakikisha afya za Watanzania na mazingira vinalindwa na pia kukuza biashara.

Alisema tangu kuanzishwa kwake hadi leo ( Novemba 30) TBS kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanikiwa kuandaa viwango zaidi ya 4,000.

"Viwango hivi ni pamoja na vile vinavyobainisha matakwa ya usalama, matakwa ya utengenezaji, matakwa ya matumizi pamoja na kanuni za upimaji vyote vikiwa na lengo la kuboresha bidhaa na huduma," alisema Dkt. Ngenya.

Alisema kwa takwimu wataalamu hao kwa mwaka huandaa, kupitia na kurejea viwango zaidi ya 500.

"Kazi hii hufanywa kwa kujitolea muda wao na kushirikiana na maofisa viwango na wadau wengine hakika shirika linatambua mchango wao mkubwa," alisema Dkt. Ngenya.

Alisema kwa kuwa wanaelekea katika Maadhimisho ya Siku ya Viwango Afrika (ARSO) Machi, mwakani ARSO imejikita kuhuwianisha viwango barani Afrika yenye lengo la kupunguza vikwazo vya kiufundi ili kuimarisha biashara kati ya nchi za Afrika.