Katika mikakati wa kuendelea kutafuta fursa za wanachama na kupanua wigo wa ushirikiano,      Uongozi wa Chama cha Wamiliki wa Viwanda Vidogo na Wazalishaji Wadogo Tanzania (TASSIM) umeweza kutembelea Shirika Binafsi la Maendeleo ya Kilimo Tanzania (Private Agricultural Sector Support-PASS TRUST) lililopo Jijini Dar es Salaam. Shirika la PASS ni Shirika lisilo la kiserikali linalodhaminiwa na Serikali ya Denmark, ambalo lipo kwa lengo la kukuza maendeleo ya sekta ya kilimo. 

Katika ziara hiyo iliyoongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa TASSIM, ndugu. E. J Mlay akiambatana na wajumbe kadhaa, waliweza kupokelewa na wenyeji wao wakiongozwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara ya PASS, Ndugu Adam Kamanda. 

Wakianza majadiliano yaliyoanza kwa utambulisho mfupi wa PASS, kazi zake na mafanikio yake hapa Tanzania ambavyo Taasisi hii imeweza kuwasaidia watanzania walio katika sekta hii ya Kilimo kwa thamani ya dollar trilioni 1.5 kuanzia mwaka 2012 hadi huu wa 2024. Kiasi hiki cha mabillioni ya shilingi kimewezesha watanzania wengi hasa wanawake na vijana ambao ndiyo kipaumbele kwenye kutengeneza fursa za ajira, uzalishaji bora wa bidhaa, uwezeshaji wa upatikanaji wa pembejeo na utoaji wa mafunzo ya kilimo na biashara.

Majadiliano yalifanyika kwa mapana zaidi ambapo uongozi wa TASSIM ukiongozwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO), Ndugu. Eliamlisi J Mlay pamoja na kuwasilisha salaamu za jumla kwa niaba ya Mwenyekiti, Ndugu. Masoud Kipanya na wanachama wote wa TASSIM, pia alitumia fursa hiyo kuielezea taasisi misingi na malengo ya TASSIM na matarajio ya ushirikiano wa baina ya hizi taasisi mbili.
      
Baada ya uwasilisho huo kufanyika, uongozi wa PASS TRUST ulifurahia ujio huo na kutoa shukrani kwa jinsi taasisi yao ilivyoweza kuonwa kwa jicho la kipekee na kuhesabika kama mdau muhimu wa TASSIM. Aidha, walieleza vile ambavyo zaidi ya asilimia tisini ya wanachama wa TASSIM wanaweza kuwa kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo moja kwa moja ambalo ndio eneo husika la uwezeshaji wa Shirika la PASS. 

Katika kutamatisha majadiliano hayo, taasisi hizi mbili za TASSIM na PASS wote kwa pamoja wameridhia kushirikiana kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo; -
                                                            
Kushirikiana katika kusimamia mafunzo, makongamano, warsha na mikutano mbalimbali kama vile Maonesho ya MADE IN TANZANIA.

Kushirikiana kwenye tathmini na uwezeshaji wa mikopo kwa wanachama wa TASSIM.

Kutembelea wanachama kwenye shughuli zao za biashara na Kilimo.

Kutoa utaalam na ushauri wa kibiashara na Kilimo.

Kufanya shughuli mbalimbali za utafiti katika sekta ya Kilimo.

Kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kukuza Kilimo.

Kushirikiana kwenye fursa mbalimbali kama miradi na programu mbalimbali zitakazoendeshwa baina ya taasisi hizi mbili.

Taasisi hii ya PASS tayari imeweza kupanua wigo wake wa kiutendaji na kusambaa nchi nzima kwa kuweza kuwa na ofisi za kikanda ikiwemo; Ruvuma, Mwanza, Mbeya, Tabora, Morogoro, Arusha na Dar es Salaam. 

Kwa namna ya kipekee, wanachama wa TASSIM wameombwa kutumia fursa hii ili kuweza kupata uwezeshwaji na kutembelewa kwenye maeneo yao ya kazi popote watakapokuwa kwa ajili ya kupata mafunzo na utaalamu elekezi.